Miaka minane iliyopita nilikutana na Haji Noorah Mwanza. Ilikuwa ni katika miaka yangu ya mwanzo mwanzo ya kama mtangazaji wa Radio Free Africa. Bado nilikuwa bwana mdogo kiumri na hata kwenye kazi hiyo ambayo mmoja wa walimu wangu wa chuoni Father Mfumbusa alikuwa akiidharau sana. ‘Kazi ya utangazaji redio ni ya ajabu sana, unajifungia kwenye kichumba unaongea peka yako,’ Mfumbusa alikuwa akisema mara kibao.
image
Ni kweli utangazaji ndivyo ulivyo lakini naapa nilipokuwa nikijifungua studio na kuanza kupiga mayowe peke yangu, nilijihisi kama dunia yote ni yangu. Niliipenda kazi ile na kwa wanaokumbuka masikio yao hayakuwadanganya jinsi nilivyosikika nikifurahia.
Mwaka 2007/08 Noorah alikuja Mwanza na hicho kilikuwa ni kipindi ambacho ukiambiwa umtaje rapper mwenye swagga na style kali za kuchana, ulikuwa huachi kumtaja Ngwair na Noorah. Si ajabu hasa ukizingatia kuwa wote walikuwa members wa Chamber Squad aka East Zoo.
Hivyo nakumbuka rafiki yangu Kidboy alimpeleka Noorah kwake kulipokuwa na studio za Tetemesha maeneo ya Kilimahewa. Kwenye gari ndogo tuliyokuwa tumepanda, kulikuwa kunachezwa wimbo wa msanii wa Canada mwenye asili ya Lebanon aliyetamba enzi hizo, Massari na wimbo wake Real Love. Noorah alikuwa akiuimba wimbo huo kwa kila mstari kama wake vile na kukibaini kipaji chake kingine cha kuimba.
Kwangu mimi na uanagenzi niliokuwa nao ilikuwa ni siku ya dhahabu kupanda gari moja na rapper huyo wa Shy town aliyekuwa si wa kukutana naye hivi hivi miaka ile. Noorah alikuwa wa moto na hakuna rapper aliyekuwa na uandishi na style kama yake. Hilo lilimpelekea kujibatiza jina na Babastylez.
Pamoja na kuanza kupata jina kupitia wimbo wake Vijimambo, umaarufu wa Noorah ulifika kileleni kupitia wimbo Ice Cream aliomshirikisha Sumalee na kutayarishwa na marehemu Roy kupitia G Records.
Ice Cream ni wimbo mkali uliokamilika katika kila kitu huku ukijikuta ukidhania Noorah rapper aliyeingia studio straight kutoka mtoni. Wimbo huo ulikuwa miongoni mwa nyimbo za kwanza kwanza za Bongo Flava zilizokuwa na video kali.
Mashairi yake aliyokuwa akiyanakshi kidogo na maneno ya Kiingereza yalimfanya Noorah arap katika mtindo uliokuwa mbele ya wakati huo. Ni rap ambayo leo hii akiingia studio na akarudia kile kile, bado tungeendelea kumwelewa na angeendena na maisha ya leo.
Idea za Noorah zilikuwa pasua kichwa na kwa rapper wa kawaida asingeweza kuzifanikisha. Ngoma kama Ukurasa wa Pili na yale majibizano na msichana anayemtaka, yatakufanya usiishie tu kucheka bali ujiulize ‘hivi huyu jamaa aliwaza nini? Alikuja kudhihirisha kuwa yupo mbele ya wakati tena na kupigia mstari uwezo wa style kwa wimbo wake Baba Style uliojaa ufanisi wa hali ya juu kiuandishi.
Sikiliza verse yake kwenye wimbo ‘Chochote Popote’ alioshirikishwa na K-Lynn. Na pengine Noorah aliamua kukomesha kabisa pale alipoalikwa na Mwana FA kwenye Unanitega. Kwa mara nyingine tena wawili hao walikuwa mbele ya wakati.
Ujuzi wa mitindo na ubunifu wa mawazo katika nyimbo zake uliendelea kudhihirika kwenye ngoma zake zingine ukiwemo Lugha Gongana ulioanzisha ukaribu wake na B’Hits. Hapo palizaliwa pia ngoma ambayo bahati mbaya haikufanya vizuri sana lakini kama ukiweza kuisikiliza leo utagundua kuwa ilikutanisha rappers wawili wenye style moto kuwahi kutokea.
Chambervernment iliwakutanisha Ngwair na Noorah na mdundo ukasimamiwa na Pancho Latino. Kwangu mimi hiyo ni moja ya ngoma kali zaidi za rappers wawili wanaojibizana baada ya Ingekuwa Vipi ya Mwana FA na Jay Moe.
Sasa swali na msingi ni kama Noorah alikuwa mbele ya wakati, wakati sasa umefika mbona tunajifanya hatumkumbuki? Kama game linavyowafanyia pioneers wengi wa Bongo Flava, ndivyo Noorah anafanyiwa pia. Katika kipindi hiki ambacho walau sasa nyimbo zake zimefika katika wakati wake, Noorah alipaswa kuwa mmoja wa rappers ambao si tu wanasikika na kuzungumziwa sana, bali pia wanaofanya show kila weekend.
Miaka ya hivi karibuni rapper huyo alipitia majaribu mengi ikiwa pamoja na kufanyiwa upasuaji mkubwa uliomfanya arudi kwao Shinyanga, kufiwa na aliyekuwa mke wake hadi kuwapoteza washkaji zake wa karibuni Ngwair na Mez B.
ara ya mwisho namsikia Noorah bado alikuwa na uwezo mkali wa kurap na ambaye mtindo wake ungekuwa na biashara zaidi kwa sasa. Kama walivyo rappers wengine wa kitambo, alijaribu kuachia ngoma mbili tatu na zikaishia kuguswaguswa, kitu kilichomkatisha tamaa na kuamua kutulia kwanza kuusoma mchezo.
Bado ninaamini kuwa Noorah ni msanii mkali na wakati wake wa ndio huu sasa japo kwa Tanzania kuishi mbele ya wakati wakati mwingine hugeuka kuwa mkosi badala ya kuwa baraka.
SOURCE:BONGO 5
Home / Uncategories / Noorah alikuwa mbele ya wakati, wakati umefika mbona tunajifanya hatumkumbuki?
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment