A TOWN BOYS ARUSHA

HATUA HII YA KENYA ITAIMARISHA EAC

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe akimsindikiza  mgeni wake Waziri mwenza wa Kenya, Amina Mohammed baada ya waziri huyo kumaliza  kuzungumza na waandishi wa habari Dar Salaam.

Hotuba ya Rais Kikwete ilifikisha ujumbe kule kulikotarajiwa. Ikiwa ni siku nne baada ya Rais kulihutubia Bunge akilalamikia nchi hizo kuitenga Tanzania, Kenya imemtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje, Amina Mohamed kuja hapa nchini kuwasilisha ujumbe wa Rais Uhuru Kenyatta kwamba nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania kwa kutambua umuhimu wake kama moja ya waanzilishi wa Jumuiya hiyo

Bila shaka hakuna Mtanzania hata mmoja ambaye hakuipongeza hatua ya Serikali ya Kenya kutuma ujumbe wa kuunga mkono msimamo wa Tanzania wa kutojitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), licha ya nchi za Uganda, Kenya na Rwanda kufanya mikutano kujadili mipango na masuala yanayohusu jumuiya hiyo pasipo kuihusisha Tanzania, kinyume kabisa na Mkataba wa Jumuiya hiyo.
Tanzania ilipinga kwa nguvu zote hatua ya nchi hizo kuitenga hata katika masuala yaliyo chini ya jumuiya hiyo, ambayo kwa mujibu wa mkataba huo yanapaswa kujadiliwa na kutekelezwa kwa pamoja na nchi zote wanachama. Rais Jakaya Kikwete alilazimika kulihutubia Bunge wiki iliyopita na kuelezea kwa kirefu ukiukwaji wa mkataba huo na athari za kuzitenga Burundi na Tanzania katika mikutano inayojadili masuala ya EAC.
Pamoja na kuzikosoa na kuzilaumu vikali nchi hizo tatu kwa kukiuka mkataba huo pamoja na itifaki zake mbalimbali, Rais Kikwete aliweka wazi msimamo kwamba Tanzania kamwe haitajitoa katika Jumuiya hiyo na itaendelea kuwa mshirika mwaminifu wa Jumuiya hiyo pasipo kutetereka. Msimamo huo bila shaka uliondoa hofu iliyokuwa imetanda miongoni mwa wananchi katika nchi zote wanachama wa EAC, kwamba Tanzania ingejitoa katika Jumuiya hiyo kutokana na kutengwa na nchi hizo tatu zilizokuwa zikiunda kile kilichoitwa ‘Coalition of the willing’ (Ushirikiano wa wenye hiari).
Hotuba ya Rais Kikwete ilifikisha ujumbe kule kulikotarajiwa. Ikiwa ni siku nne baada ya Rais kulihutubia Bunge akilalamikia nchi hizo kuitenga Tanzania, Kenya imemtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje, Amina Mohamed kuja hapa nchini kuwasilisha ujumbe wa Rais Uhuru Kenyatta kwamba nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania kwa kutambua umuhimu wake kama moja ya waanzilishi wa Jumuiya hiyo. Waziri huyo alisema kuwa, kuja kwake hapa nchini kunafuatia Serikali ya Kenya kusoma kwa undani hotuba ya Rais Kikwete ambayo alisema, ilikuwa nzuri na ilitolewa kwa nia njema tu ya kuimarisha Jumuiya hiyo na siyo kuidhoofisha.
Sisi tunadhani hatua ya Kenya ya kutafuta maridhiano na Tanzania ni ya kupongeza, hasa tukitilia maanani ukweli kwamba moja ya sababu kubwa zilizosababisha kuvunjika kwa EAC mwaka 1977 ilikuwa ni kutokuwapo utamaduni wa nchi wanachama kujikosoa na kuona umuhimu wa kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo. Hatua hiyo ya Kenya yafaa iwe mfano kwa nchi nyingine ndani ya Jumuiya hiyo, kwamba zijisahihishe pale zinapojiridhisha kwamba zimekosea hapa au pale.
Hapa hatuna maana kwamba Tanzania haikuchangia lolote katika kufikiwa kwa hali hiyo ya kutengwa. Kwa mfano, mbali na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi imekuwa ikilalamikiwa na nchi nyingi jirani zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam. Yamekuwapo malalamiko mengi na ya muda mrefu kuhusu ucheleweshaji wa kupakua na kupakia shehena za mizigo, ukubwa wa tozo za bandari na barabara pamoja na uchakachuaji wa mafuta. Ndiyo maana baadhi ya nchi hizo zimeamua kutumia Bandari ya Mombasa.
Ni matumaini yetu kwamba nchi wanachama wa EAC zitachukulia mvutano uliokuwapo kati yao na Tanzania kama changamoto ya kuzisukuma kushirikiana zaidi ili kujenga Jumuiya yenye nguvu kubwa kiuchumi. Wakati huohuo, hatua hiyo ya Kenya ni ya kijasiri, siyo udhaifu.
.



Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment