Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akitoa heshima za mwisho
kwa mwili wa Dk Sengondo Mvungi aliyefariki dunia Novemba 12, nchini
Afrika Kusini, katika Viwanja vya Karimjee Dar es Salaam jana. Kulia ni
Waziri Mkuu mstaafu
Kwa ufupi
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal
aliwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo Rais mstaafu, Benjamin Mkapa,
mawaziri wakuu wastaafu, mawaziri, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa
na viongozi wa dini, kuuaga mwili wa Dk Mvungi kwenye Viwanja vya
Karimjee, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Simanzi na vilio jana vilitawala
wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Dk Sengondo Mvungi aliyefariki dunia kwenye Hospitali ya Milpark
nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu.
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal
aliwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo Rais mstaafu, Benjamin Mkapa,
mawaziri wakuu wastaafu, mawaziri, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa
na viongozi wa dini, kuuaga mwili wa Dk Mvungi kwenye Viwanja vya
Karimjee, jijini Dar es Salaam.
Watu wengi waliowasili katika viwanja hivyo saa
3:00 asubuhi walionekana wenye huzuni, huku wakikaa katika makundi
wakizungumza kwa sauti za chinichini.
Ilipofika saa 4:00 asubuhi, mvua ilianza kunyesha
na kuwalazimisha watu waliokuwa wametawanyika katika eneo hilo kuanza
kutafuta sehemu ya kujificha.
Dakika tatu baadaye wakati mvua ikiendelea
kunyesha, gari lililokuwa limebeba mwili wa Dk Mvungi liliwasili kwenye
viwanja hivyo, kitendo kilichowafanya baadhi ya waombolezaji kuanza
kutokwa machozi.
Mara baada ya mwili kuwekwa sehemu iliyokuwa
imeandaliwa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa
Paramagamba Kabudi alipanda jukwaani kusoma historia ya marehemu.
Kabudi alisema Dk Mvungi alikuwa mtu aliyechukia
rushwa na kuheshimu utawala bora, na kwamba kifo chake kimewaunganisha
pamoja watu wa itikadi tofauti.
Aliongeza kuwa kutokana na uzalendo aliokuwa nao
kwa nchi yake, Dk Mvungi alipomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT), baada ya kumaliza elimu ya sekondari, aliendelea kuvaa magwanda
hayo alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi yalipochakaa.
Aliongeza kuwa, Dk Mvungi ambaye pia alikuwa
mwanasheria maarufu nchini, alishiriki kubadilisha mfumo wa masomo ya
sheria vyuo vikuu baada ya kuanzisha utaratibu wa kusoma shahada ya
sheria kwa miaka minne tofauti na mitatu ya awali.
“Mwaka 1998 aliitisha kikao mjini Arusha na
kushawishi kubadili shahada ya sheria kutoka miaka mitatu ya awali hadi
minne ya sasa,” alisema.
Akizungumzia uamuzi wa Dk Mvungi kugombea kiti cha
urais mwaka 2005, Kabudi alisema kwamba Mvungi hakugombea kiti hicho
kwa sababu alikuwa anajua angeshinda au alikuwa anamchukia rais
aliyekuwa madarakani wakati huo, bali alitaka kushiriki ndiyo maana
aliposhindwa alikuwa wa kwanza kukubali matokeo.
Akiongoza misa ya kuuaga mwili wa marehemu, Padri
Monsinyori Deogratius Mbiku alisema kuwa Dk Mvungi ameshakamilisha kazi
yake hapa duniani, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha anatekeleza
majukumu aliyopewa.
0 comments:
Post a Comment