Ukiombwa utoe sababu kwa nini michezo nchini imeshindwa kuleta
tija hasa katika eneo la kimataifa, bila shaka kapu kubwa litahitajika
ili kujaza sababu hizo kutokana na ukweli kwamba ziko nyingi.
Japo nizitaje chache. Hakuna uwekezaji wenye
dhamira ya dhati kuinua michezo kuanzia ngazi za chini, ambako ndiko
kwenye kiini cha vijana wengi wenye vipaji.
Nchi pia haina wataalamu wenye uwezo kubaini
vipaji vya vijana chipukizi na kuviendeleza. Makocha maalumu wa vipaji
tuliona wanabahatisha kufanya kazi hiyo.
Kadhalika, sapoti ndogo ya Serikali kusaidia sekta
ya michezo nayo ni miongoni mwa sababu. Sekta hii kila mwaka imekuwa
ilalamika kutengewa fungu dogo lisilokwenda na mahitaji husika.
Lakini pia suala la wakuu na viongozi wetu
kuingiza siasa kwenye mambo yanayohitaji utaalamu, ni tatizo kubwa
lililokosa dawa ya kulitibu. Na hili ndilo tatizo la msingi kwa nini
michezo inashindwa kusonga mbele. Viongozi wetu ni wale wale, hawana
ubunifu wameendelea kuwa watumwa wa kuongoza kwa mazoea.
Inashangaza, kwa sababu hata kama atakuja kiongozi
mpya nje ya wale wa kila siku, atakachokifanya ni kile kile. Mfumo wetu
wa uongozi umeshaharibika. Mfano mdogo. Klabu za Simba na Yanga ndizo
zinazoongoza kwa madeni ya kujitakia na baadhi yake yamezifikisha timu
hizo mahakamani, jambo ambalo ni aibu kubwa.
Klabu hizi zina utumwa wa kuwatimua makocha na
wachezaji bila kufuata taratibu na matokeo yake kujikuta zililazimika
kulipa fedha nyingi kama fidia. Tatizo ni kuongoza kwa mazoea,
alichokifanya kiongozi aliyetangulia hakiwi fundisho kwa kiongozi
anayefuata. Atafanya vile vile ilivyokuwa kwa mtangulizi wake. Nitakuwa
sahihi kusema michezo nchini haina nafasi ya kupiga hatua. Tukiendelea
kulea utamaduni wa kuwachagua viongozi kwa kufuata matakwa binafsi na
siyo mahitaji ya kukuza michezo, tusishangae kuona tunapiga hatua mbili
mbele, moja nyuma.
Kinachoshangaza ni kwamba, kuna mifano mingi ya
kimageuzi katika sekta ya michezo kimataifa, lakini viongozi wetu
wameshindwa kujifunza. Walichong’ang’ania ni siasa za majungu na fitina.
Ipo sababu wadau wa soka waseme sasa basi,
tunahitaji viongozi wabunifu watakaokuja na taswira mpya ya uongozi.
Sishawishiki kuamini kwamba hatuna viongozi wa aina hiyo, tunao wengi
katika kila mchezo.
Tatizo kubwa lililopo ni mifumo yetu ya uongozi.
Kila sehemu wamejipanga walewale, wanapokezana madaraka kama Simba na
Yanga zinavyopokezana kutwaa ubingwa Bara. Tusitosheke na dhana kwamba;
‘sikio la kufa halisikii dawa’.
0 comments:
Post a Comment