Dar/Uswisi. Kuna njia tatu ambazo Serikali ya Tanzania ikiamua
kuzitumia inaweza kurejesha mabilioni ya fedha zake ambazo zimefichwa
nchini Uswisi na kwingineko duniani, Mwananchi limebaini.
Uchunguzi ulifanywa na gazeti hili nchini Tanzania
na Uswisi unaonyesha kuwa, Mosi, Serikali inaweza kuharakisha kurejesha
fedha hizo ikiwa itatumia vyombo vyake vya dola kama vile mahakama
kutaka maelezo na majina ya walioweka fedha katika nchi husika.
Pili Tanzania inaweza kupata fedha zake ikiwa
itajiunga na Taasisi iitwayo Organization of Economic Cooperation
(OECD), ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake kurejesha fedha
ambazo zimekuwa zikihamishwa kwa njia ya ukwepaji wa kodi (transfer
pricing), na tatu ni kujiunga ‘Global Forum on Transparence and
Exchange’.
Taarifa ya 2012 ya Benki Kuu ya Uswisi (SNB)
iliripoti kuwapo kwa Sh314 bilioni kutoka Tanzania, lakini katika
taarifa yake ya mwaka jana, 2013 kiasi hicho kiliripotiwa kupungua na
kufikia Sh291 bilioni.
Dk Mark Herkenrath ambaye ni Ofisa Programu wa
Taasisi ya Alliance Sud inayojishughulisha na harakati za kupinga
uwekaji wa fedha haramu nchini Uswisi, alimwambia mwandishi wa gazeti
hili nchini humo kuwa Tanzania inaweza kuwasiliana na Serikali ya Uswisi
ikiwa inahitaji taarifa zozote kuhusu fedha zake zilizofichwa nchini
humo.
“Kama kuna ombi la kimataifa na likakubaliwa na
mamlaka ya Uswisi, taarifa zinaweza kutolewa. Serikali zinazodai kuibiwa
fedha zinapaswa kuomba zenyewe taarifa ili zipewe, lakini katika
uhalisia hili halitokei. Ni sawa na kumwomba mwizi ajitaje mwenyewe,”
Herkenrath na kuongeza:
“Kwa mfano kama kuna uchunguzi Tanzania ambao
unahusisha watu na ushahidi ukapatikana, Uswisi iko tayari kusaidia. Ni
kwa fedha zilizopatikana kwa njia haramu tu.”
Mkuu wa kikosi kazi cha kurejesha fedha na mali
cha Uswisi, Pascale Baeriwyl akizungumza na mwandishi wa Mwananchi mjini
Bern, alisema Tanzania inaweza kurejesha fedha zake kama Serikali
itakuwa na nia ya dhati ya kufanya hivyo.
“Hadi sasa Uswisi imesharudisha Dola za Marekani
1.8 bilioni kwenye nchi zilizotoka,” alisema Baeriwyl na kuongeza:
“Zinaitwa fedha za watawala (potentate funds) ambazo huwekwa kwenye
taasisi za nje za fedha. Uswisi inayo mikakati ya kuhakikisha kuwa fedha
na mali haramu haziingizwi katika taasisi zake za fedha,” alisema.
Hata hivyo, Balozi Anne Lugon- Moulin ambaye ni
mkuu wa kitengo kinachoshughulikia nchi zinazozungumza Kifaransa kusini
mwa Jangwa la Sahara alisema, Uswisi peke yake haiwezekani kufanikisha
urejeshwaji wa fedha kama Serikali ya Tanzania haitatoa ushirikiano wa
kutosha.
“Uswisi peke yake haiwezi kufanikisha kazi hii
kama Tanzania haitoi ushirikiano. Ndiyo maana tunafadhili taasisi
zinazopambana na utoroshwaji wa fedha haramu na mashirika ya misaada
ambayo pia yanafanya kazi Tanzania,” alisema Moulin.
0 comments:
Post a Comment