Dar es Salaam. Chama cha Kutetea Abiria
(Chakua) kimemwomba Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kuingilia
kati suala la kuanza kwa matumizi ya mfumo mpya wa ukatishaji tiketi kwa
njia ya mtandao kwa mabasi yaendayo mikoani, kwa madai kuwa Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imekuwa chanzo cha
ucheleweshwaji wa kuanza kutumika kwa mfumo huo.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi,
mwenyekiti wa Chakua, Hassan Mchanjama alisema wadau wote wakiwamo
Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Jeshi la Polisi na Kikosi cha Usalama
Barabarani, waliridhia kuanza kutumika kwa mfumo huo unaodhaniwa
utasaidia kupunguza kero wanayoipata abiria kutoka kwa wapiga debe,
lakini cha kushangaza Sumatra haijachukua hatua ya kutoa agizo kwa wenye
mabasi kuanza rasmi kutumia mfumo huo.
Alisema adha wanayoipata sasa abiria ya
kupandishiwa nauli kiholela kipindi cha sikukuu na shule zinapofungwa au
kufunguliwa pamoja na kulanguliwa tiketi na madalali, lisingekuwapo
kama mfumo huo wa ukataji tiketi ungekuwa unatumika.
“Taboa hawana tatizo na mfumo huu, wadau wote
tulishakubaliana na katika kikao cha mwisho kilichofanyika Desemba,
mwaka jana, Sumatra ilipewa miezi mitatu ya kutathmini ili baadaye itoe
tangazo kwa wamiliki wote wa mabasi kujiunga katika mfumo huo, kitendo
ambacho hawajafanya mpaka sasa,” alisema Mchanjama.
Hata hivyo, meneja uhusiano wa Sumatra, David
Mziray alipinga madai hayo na kusema wao siyo wahusika wanaosimamia ama
kuidhinisha kampuni itoe huduma ya aina gani kwa abiria wake.
0 comments:
Post a Comment