Dar es Salaam.
Wizara ya Mambo ya Ndani imetoa ufafanuzi kuhusu ajira zilizositishwa
na kusema siyo zile zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari jana.
Jana vyombo vya habari viliandika kuwa ajira 70 za
Idara ya Uhamiaji kwa nafasi ya Mkaguzi Msaidizi Uhamiaji zilisitishwa
baada ya kuwapo na madai ya upendeleo.
Msemaji wa Wizara hiyo, Isaac Nantanga, alisema
taarifa zilizoandikwa kuhusu kusitishwa ajira 70 zilizopatikana baada ya
usaili uliofanyika Uwanja wa Taifa hivi karibuni hazikuwa sahihi.
“Ukweli ni kuwa usaili wa nafasi ya Mkaguzi
Msaidizi wa Uhamiaji ambao awali ulianzia Uwanja wa Taifa ulikwenda
vizuri hadi wakapatikana wasailiwa wa kujaza nafasi 70 za Mkaguzi
Msaidizi wa Uhamiaji. Usajili huo haukuwa na matatizo yoyote na
waliochaguliwa walitakiwa kuripoti kazini Julai 29, lakini kwa sababu
ya sikukuu sasa wataripoti baada ya sikukuu,” alisema.
Alifafanua kuwa wasailiwa waliochaguliwa kujaza
nafasi 70 za Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji hawahusiki na usitishwaji
uliotangazwa juzi na wanatakiwa kuendelea na mipango ya kuripoti kazini
kama ilivyotangazwa hapo awali.
Wasailiwa wanaohusika na kusitishwa kwa ajira zao
ni wale waliokuwa wameshiriki katika zoezi la kuajiri Konstebo na Koplo
wa Uhamiaji ambao idadi yao ni 200 na kutakiwa kuripoti Agosti 6, lakini
wameelekezwa kusubiri hadi watakapopewa maelekezo mengine.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak
Abdulwakil amesitisha ajira za Konstebo na Koplo wa Uhamiaji
zilizotangazwa na Idara ya Uhamiaji hivi karibuni.
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na tuhuma
zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa
kulikuwa na upendeleo kwa ndugu na jamaa za watumishi wa Idara hiyo.
Kutokana na hatua hiyo, Abdulwakil ameunda Kamati ndogo ya Uchunguzi itakayochunguza tuhuma hizo.
0 comments:
Post a Comment