Ni dhahiri kwamba hali si shwati tena katika nchi yetu, kinyume
na maneno au kauli nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa hata na viongozi
wetu wakiwamo wa kisiasa wa kuitaja Tanzania kuwa kisiwa cha amani,
utulivu na mshikamano.
Tunazo sababu nyingi za kuamini hivyo hasa kwa
kuangalia idadi ya matukio ya uhalifu ambayo yanazidi kujitokeza katika
miji mbalimbali nchini, hasa Dar es Salaam.
Tumeandika mara nyingi katika safu hii tukieleza
jinsi ambavyo haturidhishwi hata kidogo wala kufurahishwa na ongezeko la
matukio haya ya uhalifu ambayo yanazidi kujitokeza wakati mwingine
mchana. Kwa bahati mbaya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama likiwamo
Jeshi la Polisi, siku zote vimekuwa vikieleza mikakati yao mbalimbali ya
kupambana na uhalifu.
Hatuna shaka na uwezo wao, hasa polisi ambao
jukumu lao la msingi ni kulinda raia na mali zao. Tunaamini kuwa
wakidhamiria uhalifu utapungua kama siyo kwisha kabisa.
Ni jambo la kusikitisha kuona kwa mfano katika
jiji la Dar es Salaam, mahali ambapo hakuna shaka tunao askari wengi wa
kutosha, askari wengi wa doria, miundombinu bora na kampuni nyingi za
ulinzi, lakini ndilo linaloongoza kwa kuwa na matukio mengi ya uhalifu,
hasa wa kutumia silaha.
Tunakumbuka aliposhika wadhifa, Mkuu wa Jeshi la
Polisi (IGP), Ernest Mangu miongoni mwa ahadi zake nyingi ilikuwa ni
kupambana na uhalifu kwa akili, nguvu na utashi wake wote.
Tunachukua nafasi hii leo kumshauri IGP Mangu na
timu yake nchini kote wakae kitako, wajitathmini upya, wajiangalie kama
mbinu zao za kukabiliana na uhalifu zinatosha au la wazibadili,
waziboreshe na penye upungufu wauondoe.
Tunaamini kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanikiwa
kurudisha imani ya wananchi dhidi ya chombo hiki ambayo inapungua kama
siyo kupotea kabisa.
Tunasema, uhalifu huu wa sasa wa kisayansi,
kitaalamu unaotokea bila kificho wakati mwingine kwenye vituo kama vya
mafuta, benki au kwingineko kama kwenye maduka makubwa na kusababisha
vifo kama kile cha mtawa wa Kanisa Katoliki, Cresencia Kapuri miezi
michache iliyopita, ni mambo yanayotisha.
Kama sehemu ya jamii, hatuna budi kukumbushana
wajibu katika kujilinda dhidi ya matukio haya ya kihalifu, ingawa
tunapenda polisi wetu wabadili mbinu za kiintelijensia za kukabiliana na
uhalifu.
Tunaamini, wahalifu tunaishi nao mitaani, ni
watoto au wajukuu zetu, wengine ni waume au wake zetu na tunaishi nao
kwenye nyumba binafsi au za kupanga. Lakini ni kwa namna gani tunatoa
taarifa kwenye vyombo vya dola kuhusu mienendo ya wengine ambao
hairidhishi? Tunatambua nchi yetu inayo mifumo ya uongozi kama wa
serikali za mitaa, vitongoji na vijiji. Ni kwa namna gani mamlaka hizi
zinashiriki kuhakikisha watu wanaishi kwa amani, utulivu kama ilivyokuwa
zamani?
Pia, tunajiuliza, ile dhana ya polisi jamii na
utii wa sheria bila shurti ambayo ilianzishwa na aliyekuwa IGP, Said
Mwema imefanya kazi kwa mafanikio kiasi gani katika kukabili uhalifu
ambao unazidi kuongezeka katika jamii yetu?
Haya ni baadhi ya maswali ya msingi ambayo tunataka yajibiwe na kila mmoja wetu katika harakati zetu za kupambana na kutokomeza uhalifu. Tunaamini tunaweza.
Haya ni baadhi ya maswali ya msingi ambayo tunataka yajibiwe na kila mmoja wetu katika harakati zetu za kupambana na kutokomeza uhalifu. Tunaamini tunaweza.
0 comments:
Post a Comment