A TOWN BOYS ARUSHA

LOWASSA:BOMU LA AJIRA KWA VIJANA KULIPUKA MUDA WOWOTE

Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema vijana 10,500 waliojitokeza hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufanya usaili wa nafasi 70 za kazi katika Idara ya Uhamiaji, ni ishara kuwa bomu la ajira litalipuka muda wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya Viwanja vya Bunge, Lowassa alisema Serikali ni lazima ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini.
Wasomi hao wa fani mbalimbali walijitokeza katika uwanja huo Ijumaa iliyopita, kuanzia saa 12 asubuhi wakisubiri kufanyiwa usaili huo.
Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la ajira na akisema ni bomu linalosubiri kulipuka.
Mbunge huyo wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia kwenye malumbano makali na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka kuhusiana na suala la ajira kwa vijana.
Kabaka akiwa bungeni, Machi 21, 2012 alitoa takwimu za namna Serikali ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye alikuwa ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana.
Jana, Lowassa kuongezeka kwa makundi ya vijana wanaopora watu katika maeneo mbalimbali nchini ni ishara ya ukosefu wa ajira. “Watanzania sasa tupo milioni 48 na kila mwaka vijana zaidi ya 30,000 wanahitimu vyuo vikuu na kazi hakuna, pamoja na hilo hatuambiwi ni vijana wangapi ambao hawana kazi,” alisema Lowassa.
Alisema lazima Serikali itengeneze ajira kwa wananchi wake, huku akimtolea mfano Rais wa Marekani, Barack Obama kwamba alishinda awamu ya pili kwa sababu ya kutengeneza ajira.
“Mfano mzuri ni katika uanzishwaji wa viwanda. Tunapofikiria kuanzisha kiwanda cha pamba kwanza lazima tuangalie tutatengeneza ajira ngapi,” alisema.
Katika kuonyesha kuwa ajira sasa ni tatizo nchini, juzi jioni wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu, Naibu Spika Job Ndugai alisema Mtanzania mwenye nia ya kugombea urais mwaka 2015 ili aweze kuelekewa kwa wananchi ni lazima aeleze mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na vyuo vikuu. Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za mwisho za Serikali ya awamu ya nne, wale wanaojipanga kwa awamu ya tano kama hawataongelea ajira basi waandike wameumia.”
Ndugai alisema vijana wasio na kazi ndiyo wapigakura wakubwa na kusisitiza kuwa mgombea yeyote makini ni lazima afikirie suala la ajira kwa vijana.Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema: “Vijana 10,500 kufanya usaili wa nafasi 70 ni janga la taifa. Yupo kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliwahi kulizungumza hili lakini akapondwa kwamba anazungumza mambo kwa kuzua. Sasa huu ndiyo ukweli wenyewe.”

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment