Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (kulia), akimjulia hali
aliyejifungua watoto pacha katika Hospitali ya Mwananyamala, Mwamvita
Kilasi wakati waziri huyo alipokwenda hospitalini hapo kutoa misaada
mbalimbali katika wodi ya watoto. Waziri huyo alikuwa akisheherekea siku
yake ya kuzaliwa
Dar es Salaam. Sakata la ufisadi wa Sh306
bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow limewang’oa wafanyakazi saba wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wafanyakazi hao wamesimamishwa kazi ikiwa ni
mwendelezo wa utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge kuhusu ripoti ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu kashfa hiyo.
Wengine ambao tayari wameshawajibika katika kashfa
hiyo ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
aliyejiuzulu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka aliyefukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliyesimamishwa kupisha
uchunguzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba alisema pia Serikali imetoa siku 30 kwa
walionufaika na mgawo wa mamilioni ya fedha kutoka kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering Ltd, James Rugemalira kulipa kodi
kulingana na kiasi walichopokea.
Hatua TRA
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kwa wafanyakazi
wa TRA waliohusika na sakata hilo Nchemba alisema; “Mpaka sasa
wafanyakazi saba wamesimamishwa kazi ili kupisha vyombo vinavyohusika
viweze kuchukua hatua zaidi na mimi nilikuwa nasema wachukue hatua zaidi
kwa kuwa haiwezekani badala ya Dola milioni 20 mtu anaweka fedha za
Tanzania Sh20 milioni, hii ni makusudi au njama za kutekeleza wizi huo.
“Ukisema ulikuwa unajua ni njama, hivyo hustahili
kuwapo na ukisema ulikuwa hujui pia hustahili kuwapo. Huwezi kusomeshwa
kwa kodi ya Watanzania halafu unapopewa fursa ya kusimamia makusanyo ya
kodi ukafanya unavyojua,” alisema Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba
Magharibi (CCM).
“Mtu hawezi kuiba Sh30 bilioni halafu ukamfukuza
kazi pekee, hii utakuwa unampa likizo ya kwenda kutumia fedha hiyo,
ifike mahali mtu anapoiba anafilisiwa mali zake ili kuwa fundisho kwa
wengine.”
Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM
(Bara) alisema kitendo cha mtumishi wa umma kufanya vibaya na kisha
kuhamishiwa sehemu nyingine haitakiwi kuwapo kwa kuwa hiyo ilikuwa
inatokea wakati watumishi wakiwa wachache.
“Unajua zamani unakuta wahandisi ni wachache
unapomfukuza moja kwa moja unakosa wa kukaa nafasi hiyo lakini sasa
watumishi na wataalamu ni wengi mtu akikosea ni kumwondoa akatafute kazi
sehemu nyingine kwani hatutakiwi kufumbia macho vitendo hivi,” alisema
Nchemba.
Waliopata mgawo
Kuhusu walionufaika na mgawo huo, Nchemba alisema
“TRA imeshawatumia fomu za mahesabu ya kodi wanazotakiwa kulipa na wao
sasa wakae na wahasibu wao waseme wanatakiwa kulipa kiasi gani ndani ya
siku 30 kuanzia Januari Mosi mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment