Ule msemo wa kazi nzuri ukiwa hujaipata na huwa mbaya ukiwa
nayo, unaweza ukaonyesha uhalisia wakati unapopaswa kufahamu ni aina ipi
ya mkataba wa ajira uliosainiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa.
Aina ya mkataba wa ajira huonyesha mustakabali wa
ajira yenyewe, humpa mfanyakazi na mwajiri fursa ya kufahamu haki na
wajibu wa kila upande na hivyo kujenga mazingira mazuri ya utekelezwaji
wake kwa kulinda masilahi ya kila upande.
Mkataba wowote ule unaoingiwa kati ya pande mbili,
ni lazima uwe na vigezo vikuu vya mkataba ikiwamo makubaliano ya pande
mbili, malipo halali, lengo halali, uwezo wa kuingia mkataba na hiyari.
Bila kujali ni aina ipi ya mkataba wa ajira
mliosaini, kama kimojawapo kati vigezo vikuu vya uhalali wa mkataba
kitakosekana, kinaweza kuufanya mkataba wenyewe kuwa batili tangu
mwanzo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha sheria ya ajira
na uhusiano kazini ya mwaka 2004, mikataba ya ajira iko ya aina tatu
ambayo ni; mkataba usiokuwa na muda maalumu, mkataba wa muda maalumu kwa
wataalamu na kada ya uongozi pamoja na mkataba wa kazi maalumu.
Mkataba usiokuwa na muda maalumu ni ule ambao
unasainiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa, ambao unaweza kuonyesha tarehe
uliyosainiwa lakini hauonyeshi au hauelezi kuwa utaisha lini. Mikataba
ya namna hii mara nyingi huwa katika taasisi za umma na baadhi ya
taasisi binafsi.
Aina ya pili ya mkataba wa ajira ni mkataba wa
muda maalumu kwa kada ya uongozi. Aina hii ya mkataba huhusisha zaidi
kada ya uongozi au mwajiriwa mwenye fani ya aina fulani ambaye huajiriwa
kushika wadhifa fulani wa juu katika utekelezaji wa majukumu yake. Hata
hivyo aina nyingine za waajiriwa wanaweza pia kuwa na mkataba wa muda
maalumu bila kujali kada anayotoka kulingana na mahitaji maalumu ya
mwajiri.
Aina ya tatu ya mkataba wa ajira ni mkataba kwa
kazi maalumu. Mkataba huu unaweza kupewa kipindi maalumu cha kumalizika
au mara nyingi kumalizika kwake hutegemea kumalizika kwa kazi husika
ambazo mwajiri na mwajiriwa watakuwa wamekubaliana kutekeleza.
Hii yaweza kuhusu utekelezaji wa mradi fulani au
shughuli maalumu ambayo kuisha kwake ndiyo huashiria kufikia mwisho kwa
mkataba wa ajira.
Jambo la muhimu na la kuzingatia ni kwamba kifungu
cha 15 cha sheria ya ajira na uhusiano kazini, kinamtaka kila mwajiri
na mwajiriwa kuhakikisha kuwa kabla ya kuanza kazi, kuna mkataba wa
maandishi uliosainiwa kati ya pande hizo mbili.
Mkataba ndiyo utakaoeleza aina ya shughuli
utakazofanya, mipaka, unawajibika kwa nani, malipo yako, haki zako za
msingi, namna ya kuvunja mkataba na masuala mengine muhimu ambayo
hamuwezi kukubaliana tu kwa maneno.
Tatizo kubwa la mkataba wa maneno ni ugumu wa
kuuthibitisha. Kukosekana kwa mkataba wa maandishi kunahatarisha ulinzi
na usalama wa haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa. Usikubali kuanza
kazi bila mkataba.Usikubali kusaini mkataba bila kuusoma na kuuelewa pia ni muhimu kujua
umeingia mkataba wa aina gani kati hizo aina tatu nilizoeleza hapo juu,
ili ujue haki na wajibu wako kisheria na namna gani maslahi yako kama
mwajiri au mwajiriwa yanaweza yakalindwa pasipo vikwazo vya aina yoyote.
0 comments:
Post a Comment