Watu wengi hawajui kuwa kupitia simu yako ya mkononi, tabiti, au
kompyuta yenye mtandao, unaweza kununua bidhaa zako na kuzipata kwa
muda mfupi mlangoni kwako.
Kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (Tehama) imefungua milango ya kununua bidhaa mtandaoni kwa
kuyavuta maduka na kupunguza utegemezi wa kununua bidhaa kwa kuonana na
muuzaji.
Kampuni kadhaa za nje na za ndani kama Kaymu,
Hellofood, Kivuko, Jumuia, ShoppingTz na nyinginezo, zimeanzisha huduma
hiyo ili kutumia fursa adhimu ya biashara katika jamvi la Tehama.
Biashara hii inafanyikaje?
Katika soko au duka la mtandaoni, mteja na muuzaji
hawakutani ana kwa ana, bali kupitia mtandao kwa kuunganishwa kupitia
tovuti au programu ya simu (‘app’) ambazo nyingi humilikiwa na kampuni
za kijasiriamali.
Tovuti hizo huwa ni jamvi au meza ambazo wauzaji
huweka taarifa zao za kina kama vile bei na aina ya bidhaa, idadi,
kiwango, mwaka wa kutengenezwa (kwa bidhaa za kuisha muda) na uwezo
wake.
Taarifa hizo huambatana na picha halisi za bidhaa
ili kuzuia utata unaoweza kutokea mteja anapokuta bidhaa aliyonunua na
kuletewa siyo ile iliyopo pichani. Programu ya kompyuta inayofanya kazi
kama kikapu hutumika kufanikisha ununuzi kwa kumjulisha mnunuzi jumla ya
bidhaa alizonunua na fedha anazodaiwa.
Katika tovuti hizo kuna kila aina ya bidhaa
kuanzia nguo, vyakula, magari, vitabu, vifaa vya elektroniki, vipodozi,
vidani, muziki, video na vinginevyo.
Malipo
Malipo katika biashara hiyo iliyoanzishwa miaka 35
iliyopita na mjasiriamali Mwingereza Michael Aldrich, yanaweza
kufanyika moja kwa moja mtandaoni au wakati mteja anapopokea bidhaa.
Meneja Mkuu wa kampuni ya kuuza chakula mtandaoni,
Sherrian Abdul anasema wateja wanaweza kulipia kupitia Tigo Pesa (kwa
sasa) au kulipia wakati wanapokea chakula.
Pia, shoponlinetz kupitia tovuti yao wamebainisha
kuwa wateja wanaweza kufanya malipo yao kupitia kampuni za malipo za
Visa, Visa Electron, Paypal, Mastercard, Airtel Money na Tigo pesa.
Bidhaa kama muziki na video au programu za kompyuta unaweza
kuzipakua haraka mara tu baada ya kuzilipia, wakati bidhaa kama nguo na
nyinginezo zitakuhitaji usubirie kidogo inatokana na umbali wa duka
lilipo na makazi yako.
Changamoto za usafirishaji bidhaa
Pamoja na mfumo wa kielektroniki kufanya miamala
ya biashara husika mtandaoni kwa haraka, usafirishaji wa bidhaa hadi kwa
wateja umekuwa ukikumbwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa anuani za
makazi. “Mara nyingi tunajitahidi kupata taarifa za msingi alipo mteja
jinsi iwezekanavyo, mara nyingi tunaangalia mwanzo wa mtaa au kituo cha
basi.
Ila tunategemea sana kampuni bora za usafirishaji
kukamilisha zoezi hilo ambazo huwapigia wateja na kuwapelekea wateja
bidhaa ndani ya muda unaotakiwa,” anasema Mkuu wa masoko na uhusiano wa
Kampuni ya Kaymu, Angaza Nkurlu.
Hata hivyo, gharama za usafirishaji zinatofautiana
kutokana umbali na ukubwa unaosafirishwa, kwa Kaymu bei hizo ni kati ya
Sh3,000 hadi 4,000 kwa bidhaa ndogo ndogo na umbali wa kawaida wakati
Hellofood ni kati ya Sh2, 000 hadi Sh3, 000.
Mustakabali wa biashara
Mtaalamu wa Tehama, Jumanne Mtambalike anasema
biashara hiyo inakuwa kwa kasi huku kampuni za kimataifa kama Kaymu na
Jumia zikibisha hodi nchini na kampuni za kizawa za Kivuko, Online
Shopping na Gateway na nyingine nazo zimeonyesha ushindani mkubwa.
“Unajua kati ya mwaka 2011 hadi 201,3 biashara za aina hiyo zilikuwa
zinafanyika kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook kwa muuzaji kuweka
bidhaa anayouza kwenye ukurasa wake au wa kundi na kuweka mawasiliano
ili wateja wanaohitaji wamtafute.
“Lakini mwaka huu tumeshuhudia tovuti lukuki
maalumu kwa biashara hiyo na kwa taarifa nilizopatiwa hivi karibuni,
mtandao wa Kaymu Tanzania unafanya biashara na watu zaidi ya 1,000,”
anasema.
Licha ya biashara hiyo kukua kwa kasi nchini,
baadhi ya wananchi kama Thabiti Ibrahimu hana uhakika kwamba ununuaji wa
bidhaa mtandaoni una usalama wa kutosha hususan kwenye malipo.
Matukio ya wizi wa mtandao kupitia mashine za
kutolea fedha au fedha kupitia njia ya simu, anasema yanazidi kumpa hofu
iwapo kweli atapata bidhaa yake ikiwa salama.
Hata hivyo, Mtambalike anasema ni lazima wengi
wapate hofu kutokana kutomjua mtu anayewauzia, huku akiwatoa wasiwasi
katika upande wa malipo kwa kuwa maduka mengi yanataka ulipe wakati
unapokea bidhaa hivyo unaweza kuikataa iwapo umeletewa usiyoihitaji.
“Kwangu mimi vikwazo vikubwa ni vitatu: uelewa
mdogo wa watu kuhusu biashara za mitandao, ukosefu wa mfumo ulio imara
wa malipo na wenye ulinzi wa kutosha na usalama wa taarifa za mnunuzi na
ukosefu wa mtandao baadhi ya maeneo ya Tanzania,” anasema mtaalamu
huyo.Kwa Nkurlu, changamoto zilizopo ni fursa yao kuwekeza zaidi kwa kutoa
elimu kwa wananchi namna ya kununua na kuendelea kupeana utalaamu kati
ya wasafirishaji na watoaji huduma kifedha ili kuboresha zaidi biashara
hiyo.Kwa Nkurlu, changamoto zilizopo ni fursa yao kuwekeza zaidi kwa kutoa
elimu kwa wananchi namna ya kununua na kuendelea kupeana utalaamu kati
ya wasafirishaji na watoaji huduma kifedha ili kuboresha zaidi biashara
hiyo.
0 comments:
Post a Comment